" DIWANI IWAMBI ATOA MOTISHA YA FEDHA KUCHOCHEA UFAULU WA WALIMU NA WANAFUNZI

DIWANI IWAMBI ATOA MOTISHA YA FEDHA KUCHOCHEA UFAULU WA WALIMU NA WANAFUNZI


Na Lydia Lugakila-Misalaba Media

Mbeya

Diwani wa Kata ya Iwambi mkoani Mbeya, Mhe. Gloria Ipopo Mwamajemba (Mchina), ametoa motisha ya fedha kwa walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Iwambi waliopata matokeo mazuri katika masomo yao, ikiwa ni jitihada za kuchochea ari ya kufundisha na kujifunza.

Katika mpango huo wa motisha, kila mwanafunzi aliyepata alama A amezawadiwa shilingi 15,000 kwa kila somo, huku waliopata alama B wakipatiwa shilingi 10,000. Hatua hiyo imelenga kuongeza ushindani chanya na kuhamasisha bidii zaidi kitaaluma.

Mbali na wanafunzi, walimu waliofanya vizuri pia wamepatiwa zawadi za fedha ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wao katika kuinua kiwango cha elimu shuleni hapo.

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo, Mhe. Ipopo alikabidhi vyeti pamoja na zawadi kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha pili na kidato cha nne kwa mwaka 2025/2026.

Aidha, alitoa shukrani kwa viongozi wa Jiji la Mbeya pamoja na Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Patrick Mwalunenge, kwa mchango wao katika kuendeleza sekta ya elimu.

Diwani huyo alieleza kuwa jitihada hizo ni sehemu ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika azma ya kuboresha elimu nchini, akibainisha kuwa serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuinua viwango vya ufaulu.


Alisisitiza kuwa utoaji wa motisha kwa walimu na wanafunzi ni nyenzo muhimu ya kuongeza morali, ubunifu na uwajibikaji katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.

Vilevile, aliwahimiza wazazi kushirikiana kwa karibu na walimu kwa kuwapa ushirikiano na motisha wanafunzi, badala ya kutegemea juhudi za serikali pekee.

Kwa upande mwingine, Mhe. Ipopo aliwataka walimu kuendelea kujituma ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika Kata ya Iwambi na kuifanya kuwa miongoni mwa maeneo yanayofanya vizuri kitaaluma.







Post a Comment

Previous Post Next Post