
Tanzania imepiga hatua nyingine muhimu ya kihistoria katika kuimarisha uchumi wa viwanda na biashara za kimataifa baada ya Serikali kusaini mkataba wa makubaliano na kampuni ya Panda Hill Tanzania Limited kwa ajili ya uendelezaji wa mradi mkubwa wa madini ya niobium mkoani Mbeya.
Hafla hiyo ya utiaji saini iliyofanyika jijini Mbeya, inaashiria mwanzo wa safari ya Tanzania kuelekea kuwa mzalishaji wa nne wa madini hayo adimu duniani, hatua inayotarajiwa kuongeza thamani ya rasilimali za taifa na kuifanya nchi kuwa mshiriki wa moja kwa moja kwenye minyororo ya ugavi ya teknolojia za kisasa barani Afrika, Asia, Ulaya na Marekani.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza katika hafla hiyo, amebainisha kuwa mradi wa Panda Hill ni wa kipekee kwani unahusu uzalishaji wa madini ya kimkakati ambayo hayapatikani kwa urahisi maeneo mengi duniani.
Kwa sasa, soko la niobium linatawaliwa na nchi za Brazil inayozalisha takriban asilimia 91 ya mahitaji ya dunia na Canada inayochangia asilimia sita, hivyo kuingia kwa Tanzania kutaifanya nchi kuchangia asilimia nne ya mahitaji ya dunia kupitia uzalishaji wa tani 100,000 kwa mwaka.
Mavunde amesisitiza kuwa mradi huu unaenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025-2050 na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanayotaka madini yachakatwe hapa nchini ili kuongeza thamani na manufaa kwa wananchi.
Umuhimu wa madini ya niobium unajidhihirisha katika matumizi yake kwenye teknolojia za kisasa, ikiwemo kuongeza uimara wa chuma na kutengeneza aloi za utendaji wa juu zinazohitajika kwenye miundombinu mikubwa, injini za ndege, na utengenezaji wa magari ya umeme.
Mradi huu unajumuisha ujenzi wa mgodi, kituo cha uchenjuaji, na kiwanda cha kuzalisha ferroniobium, hali inayolifanya eneo la Panda Hill kuwa kitovu cha usindikaji wa madini hayo. Aidha, mradi unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa kutoa ajira kwa zaidi ya watu 1,600 wakati wa ujenzi na ajira za kudumu 600, huku idadi ya wanufaika wa moja kwa moja na wasio wa moja kwa moja ikikadiriwa kufikia watu 7,000.
Katika muundo wa umiliki ,Serikali ya Tanzania itakuwa na hisa asilimia 16, hatua inayolenga kuimarisha ushiriki wa taifa katika maamuzi ya kimkakati na kuhakikisha faida zinapatikana kwa uwazi.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, pamoja na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, walisaini makubaliano ya wanahisa kukamilisha mfumo wa usimamizi wa mradi huo.
MWISHO
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment