" MAKALA: JUKUMU LA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA (TFS) KATIKA MAENDELEO ENDELEVU

MAKALA: JUKUMU LA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA (TFS) KATIKA MAENDELEO ENDELEVU

 

Na Mapuli Kitina Misalaba

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ni taasisi muhimu ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa The Executive Agencies Act, Sura ya 245, kwa lengo la kusimamia rasilimali za misitu na nyuki nchini kwa ufanisi na tija.

Kuanzishwa kwa TFS kulikuja baada ya mageuzi ya kisekta ambapo mwaka 2009 kulikuwepo Idara ya Misitu na Nyuki (FBD), kabla ya kuanzishwa rasmi kwa TFS mwaka 2010/11. Baadaye, majukumu yake yalipanuliwa mwaka 2018 na 2019 kwa kujumuisha shughuli za TTSA na vituo vya malikale kupitia Tangazo la Serikali Na. 269 (GN 269).

Taasisi hii inaongozwa na sera na sheria mbalimbali ikiwemo Forest and Beekeeping Policy ya mwaka 1998, pamoja na Sheria ya Misitu Sura ya 328 na Sheria ya Ufugaji Nyuki Sura ya 224.

Dira ya TFS ni kuwa kinara barani Afrika katika usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki, huku dhima yake ikiwa ni kulinda, kuendeleza na kutumia rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa ujumla, Tanzania ina takribani hekta milioni 48.1 za misitu, ambapo sehemu kubwa ipo chini ya usimamizi wa serikali za vijiji na serikali kuu. TFS pekee inasimamia misitu 464 yenye jumla ya hekta milioni 14.5, ikiwemo misitu ya asili, mashamba ya miti, mikoko pamoja na hifadhi za nyuki.

Shamba la miti la Sao Hill ni moja ya miradi mikubwa na ya kimkakati inayosimamiwa na TFS. Shamba hili lina historia ndefu iliyoanza na majaribio ya upandaji miti kati ya mwaka 1939 hadi 1951, kabla ya kuanza upandaji mkubwa kuanzia mwaka 1960 hadi 1980.

Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill - PCO Tebby Yoramu alifafanua kuwa shamba hilo lipo katika maeneo ya Mufindi mkoani Iringa na Kilombero mkoani Morogoro, na linajumuisha jumla ya misitu 13 ya hifadhi yenye eneo la hekta 135,903. Kati ya hizo, zaidi ya hekta 86,000 ni mashamba ya miti yaliyopandwa, huku sehemu iliyobaki ikiwa ni misitu ya asili na maeneo ya uwekezaji.

PCO Tebby Yoramu alisema Kiutawala shamba hilo limegawanywa katika tarafa nne ambazo ni Irundi, Ihefu, Ihalimba na Mgololo, kila moja ikiwa na majukumu ya kusimamia uzalishaji na ulinzi wa misitu.

Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill anayesimamia Mipango na Matumizi ya Rasilimali Misitu - SCO Peter Nyahende alisema shughuli zinazofanyika Sao Hill ni pamoja na: Maandalizi ya upandaji miti, Uzalishaji wa miche, usimamizi wa Bustani, Upandaji, upaliliaji (weeding), upogaji (pruning) na upunguzaji miti (thinning)

Shughuli zingine ni Ulinzi wa misitu dhidi ya moto, uvamizi, Ukusanyaji wa mapato ya serikali na Ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi ambapo Zaidi ya hayo TFS imekuwa ikishirikisha jamii zinazozunguka shamba hilo ili kunufaika kiuchumi kupitia ajira, biashara ndogo ndogo na miradi ya kijamii jambo linalochochea ulinzi wa rasilimali hizo.

Katika kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa rasilimali za misitu na fursa zake kiuchumi, viongozi na wanachama wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tawi la Tanzania (MISA TAN), ambao ni waandishi wa habari na watangazaji kutoka vyombo mbalimbali nchini, walifanya ziara mkoani Iringa kutembelea maeneo ya utalii na uzalishaji, ikiwemo Shamba la Miti la Sao Hill linalosimamiwa na Tanzania Forest Services Agency (TFS).

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James alisema kuwa mkoa huo una fursa nyingi za kiuchumi pamoja na vivutio vya utalii vinavyohitaji kutangazwa zaidi ili kuvutia wawekezaji na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko alisema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa kauli mbiu ya kongamano lao la Mwaka 2026 isemayo “Iringa Imara Itajengwa kwa Umoja na Uwajibikaji,” akisisitiza nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusu uhifadhi wa misitu na matumizi endelevu ya rasilimali.

Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki ziara hiyo akiwemo Moshi Ndugulile, Simeo Makoba, Amina Mbwambo, Kadama Malunde, Neema Nkumbi na Marco Maduhu, walieleza kuwa ziara hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu mchango wa misitu katika uchumi na umuhimu wa kuelimisha jamii juu ya uhifadhi wake.

Mbali na ziara hiyo, Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club – SPC) ilifanya ziara katika Hifadhi ya Msitu wa Lubaga maarufu kama Hashi, iliyopo mkoani Shinyanga, kwa lengo la kujionea juhudi za uhifadhi wa misitu pamoja na mchango wake katika kulinda mazingira na kukuza uchumi wa wananchi.

Siku ya Misitu Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 21 Machi, ikiwa ni jukwaa muhimu la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa rasilimali misitu katika maisha ya binadamu na maendeleo ya Uchumi ambapo Maadhimisho hayo yalianzishwa mwaka 1971 na Food and Agriculture Organization (FAO), kabla ya kuidhinishwa rasmi na United Nations mwaka 2012 na kuanza kuadhimishwa kimataifa mwaka 2013.

Kwa upande wa Tanzania, Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Katavi, Kigoma, Shinyanga na Tabora ina jumla ya misitu 33 yenye takribani hekta milioni 5.7. Misitu hii kwa kiasi kikubwa ina uoto wa miombo ambao hupatikana katika nchi chache duniani ikiwemo Mozambique, Zambia, Malawi na Democratic Republic of the Congo.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa TFS Kanda ya Magharibi, Afisa Misitu Mwandamizi na Mkuu wa Operesheni Kanda hiyo, Shadrack Msilu alisema uoto huo wa miombo ni muhimu sana kwani unachangia maisha ya zaidi ya watu milioni 100 katika ukanda huo, huku ukiwa tegemeo kubwa kwa wananchi wa Tanzania kwa zaidi ya asilimia 87 kutokana na mchango wake kiuchumi. Hata hivyo, alisema bado misitu inakabiliwa na changamoto za uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu.

Kwa mujibu wa takwimu, taifa hupoteza takribani hekta 469,000 za misitu kila mwaka, hali inayohitaji hatua za haraka za uhifadhi na kwamba katika kukabiliana na hali hiyo, Kanda ya Magharibi imeanza jitihada za kuongeza misitu kupitia maeneo ya ngitiri, hasa katika Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga.

Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania -TFS, Prof. Dos Santos Silayo alisema Misitu ni mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania na kwamba kupitia TFS rasilimali hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya viwanda, hasa vinavyotegemea malighafi za mbao na kwamba sekta hii hutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania kuanzia ngazi ya uzalishaji hadi usindikaji.

Prof. Dos Santos alieleza kuwa Misitu pia ni chanzo kikubwa cha mapato ya serikali kupitia ushuru na mauzo ya mazao ya misitu, huku ikiwezesha biashara za ndani na nje ya nchi. Mbali na hayo, misitu inalinda mifumo ya ikolojia, ikiwa ni pamoja na vyanzo vya maji na hali ya hewa.

“Umuhimu wa misitu hauishii kwenye uchumi pekee bali pia unahusiana moja kwa moja na usalama wa taifa ambapo Usalama wa kiuchumi: Hutoa ajira na kusaidia viwanda, Usalama wa mazingira: Hulinda ardhi, maji na hali ya hewa”.

“Aidha Usalama wa kijamii: Hupunguza migogoro ya rasilimali huku Usalama wa kimkakati: Huhifadhi rasilimali muhimu kwa vizazi vijavyo”.

Mkazi wa Kishapu, Sumai Salum akizungumza kwa niaba ya wananchi alisema kuwa misitu imekuwa na mchango mkubwa katika maisha yao ya kila siku, hususan katika kupata kipato kupitia shughuli kama ufugaji nyuki na uvunaji wa mazao ya misitu. 

Sekta ya misitu na nyuki inachangia takribani asilimia 3.3 ya pato la taifa moja kwa moja na hadi asilimia 15 kupitia huduma za ikolojia, jambo linaloonyesha umuhimu wake mkubwa kiuchumi.

TFS inaendesha programu mbalimbali za maendeleo, zikiwemo: Uendelezaji wa viwanda vya mazao ya misitu na kuongeza Thamani, Upanuzi wa mashamba ya miti, Udhibiti wa moto wa misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Elimu kwa umma na ushirikishwaji wa jamii, Matumizi ya teknolojia za kidijitali kufuatilia rasilimali na Kuendeleza utalii wa ikolojia.

Ufugaji nyuki ni sehemu muhimu ya shughuli za TFS, hasa katika kukuza uchumi wa vijijini. Tanzania huzalisha zaidi ya tani 30,000 za asali kwa mwaka, huku mikoa ya Tabora, Singida, Katavi na Kigoma ikiwa vinara wa uzalishaji.

Sekta hiyo hutoa ajira, huongeza kipato cha wananchi na kusaidia katika uchavushaji wa mazao ambapo tafiti zinaonyesha kuwa nyuki wanachavusha takribani asilimia 75 ya mimea inayotoa maua na asilimia 35 ya mazao ya chakula duniani.

Iwapo nyuki watatoweka: Uzalishaji wa chakula utapungua, Bei za vyakula zitapanda na Mfumo wa ikolojia utadhoofika. Hivyo basi uhifadhi wa misitu ni sawa na kulinda maisha ya binadamu.

Pamoja na mafanikio yaliyopo, TFS inakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo: Uvamizi wa misitu na matumizi holela ya ardhi, Utegemezi mkubwa wa kuni na mkaa kama nishati, Moto wa misituni, Uhaba wa watumishi, Mabadiliko ya tabianchi, Matumizi madogo ya teknolojia na Miundombinu isiyoridhisha.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, TFS imeweka mikakati ifuatayo: Kuimarisha mipango bora ya matumizi ya ardhi, Kuongeza doria na kutumia teknolojia za kisasa kufuatilia misitu, Kuanzisha na kuimarisha vikosi vya kudhibiti moto, Kuongeza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, Kutoa mafunzo kwa watumishi na jamii na Kushirikiana na vyombo vya habari kutoa elimu ya uhifadhi.

Kwa ujumla, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ni mhimili muhimu katika kulinda rasilimali za taifa na kuchochea maendeleo endelevu na kwamba kupitia usimamizi madhubuti wa misitu na nyuki, taasisi hii inaendelea kuhakikisha kuwa rasilimali hizi zinawanufaisha Watanzania wa leo na vizazi vijavyo.

Ujumbe muhimu unabaki kuwa:
“Kama misitu ni makazi ya nyuki, basi usalama wetu unaanzia msituni.”

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post