" BULIGE FC YAANDIKA HISTORIA KWA KUMUONDOA KIGOGO MWINGINE NYANDOLWA FC, YATINGA NUSU FAINALI YA NIACHEKONA CUP 2026

BULIGE FC YAANDIKA HISTORIA KWA KUMUONDOA KIGOGO MWINGINE NYANDOLWA FC, YATINGA NUSU FAINALI YA NIACHEKONA CUP 2026


Na Mapuli Kitina Misalaba

Timu ya Nyandolwa FC, inayoundwa na wachimbaji wa madini kutoka Mgodi wa Wachapa Kazi uliopo Nyandolwa, imeondolewa katika mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penati na Bulige FC katika mchezo wa robo fainali uliochezwa leo katika Uwanja wa Mwabenda, Kata ya Solwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulimalizika kwa sare ya goli 1-1 ndani ya dakika 90 za kawaida. Bulige FC ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao katika kipindi cha kwanza kabla ya Nyandolwa FC kusawazisha ndani ya kipindi hicho hicho na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare.

Baada ya dakika 90 kukamilika bila kupatikana mshindi, sheria za mashindano zilimtaka mshindi kupatikana kwa mikwaju ya penati ambapo Bulige FC ilionyesha utulivu mkubwa na kufanikiwa kupata penati 5 dhidi ya 4 za Nyandolwa FC.

Matokeo hayo yamewaacha wengi wakishangazwa kutokana na Nyandolwa FC kuwa miongoni mwa timu zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa ya kufika hatua ya fainali. Tangu kuanza kwa mashindano hayo, timu hiyo ilikuwa haijaruhusu kufungwa hata goli moja katika mechi zake zote kabla ya mchezo wa leo.

Kwa ushindi huo, Bulige FC imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya NIACHEKONA CUP 2026 na sasa inasubiri mshindi wa mchezo wa kesho ili kujua mpinzani wake katika hatua hiyo muhimu.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Katibu wa Kamati ya Mashindano, Sambayi Jilya, ametangaza kuwa mchezo wa kesho utawakutanisha Shilabela FC dhidi ya Kashishi FC katika robo fainali ya mwisho ya mashindano hayo, mchezo utakaokamilisha timu zitakazofuzu hatua ya nusu fainali.

Mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 yameandaliwa na Paul Daud Augustino maarufu MC NIACHEKONA kwa ufadhili wa Shirika la Lushu Foundation, yakilenga kuibua vipaji vya vijana, kukuza michezo na kuimarisha mshikamano wa jamii.

Kwa huduma za MC, matangazo na ushereheshaji wa matukio mbalimbali, wasiliana na MC NIACHEKONA kupitia namba 0757 267 738.

Kikosi cha Bulige FC na sabu.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post