
Tanzania imeendelea kuthibitisha nafasi yake ya uongozi katika ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika, huku nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) zikieleza nia ya kuja nchini kujifunza mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa agenda hiyo.
Pia, SADC imeipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumtambua Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri na mchango mkubwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, katika Kanda na Afrika kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ameeleza hayo wakati wa Mkutano wa Pamoja wa Kamati ya Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Nishati na Maji wa nchi wanachama wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao Julai 17, 2026.
Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza kwa mafanikio Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, ambapo matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yamefikia asilimia 28.6.
Mhe. Salome amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kimkakati, ikiwemo kutekeleza katazo la matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa siku, hatua iliyoanza rasmi Machi 23, 2023. Aidha, Serikali imetoa ruzuku kwa taasisi mbalimbali zikiwemo Jeshi la Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na shule ili kuziwezesha kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Ameongeza kuwa Serikali imezindua Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia mwezi Juni 2025 pamoja na kukamilisha utafiti wa msingi (baseline survey) utakaosaidia kufuatilia na kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa mkakati huo.
“Serikali pia imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwa matumizi ya kupikia majumbani, sambamba na utoaji wa ruzuku kwa baadhi ya vifaa vya nishati safi ya kupikia pamoja na uagizaji wa gesi ya LPG,” amesema Mhe. Salome.
Akiwahimiza nchi wanachama kuimarisha ushirikiano wa kikanda, Mhe. Salome amezialika nchi za SADC kuja Tanzania kujifunza uzoefu na mbinu zilizowezesha nchi kufikia mafanikio hayo ili kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia katika ukanda huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Umeme wa Zimbabwe, Mhe. July Moyo, amesema nchi wanachama wa SADC zinapaswa kuitembelea Tanzania ili kujifunza kwa vitendo hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, akibainisha kuwa uzoefu huo utazisaidia nchi hizo kuimarisha na kukamilisha mikakati yao ya kitaifa.
Mkutano huo wa Mawaziri wa Nishati na Maji wa SADC ulijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kikanda katika sekta za nishati na maji, huku Tanzania ikiendelea kuonesha mfano bora katika utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia barani Afrika.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254.
Post a Comment