Tanzania na Misri zimeainisha maeneo ya kipaumbele ya ushirikiano yanayolenga kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta za bandari, usafirishaji, kilimo, nishati, maji na viwanda ili kukuza biashara, uwekezaji na ajira katika nchi hizo mbili.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mheshimiwa Abdel Fattah El-Sisi, alipomtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Rais Dkt. Samia amesema uhusiano wa kihistoria kati ya mataifa hayo unapaswa kutafsiriwa katika miradi inayoonekana na yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, akibainisha kuwa kiwango cha sasa cha biashara hakiakisi ukubwa wa uchumi na fursa zilizopo.
Katika sekta ya uchukuzi, Tanzania imeikaribisha Misri kuwekeza katika uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa miundombinu ya Bandari ya Bagamoyo, ikiwemo ujenzi wa reli itakayoiunganisha na Kongani ya Viwanda ya Kwala na Reli ya Kisasa (SGR).
Pande hizo mbili zimeeleza dhamira ya kuimarisha ushirikiano katika kuunganisha bandari zao, kuanzisha huduma za usafiri wa baharini na kujenga vituo vya kisasa vya kuhifadhi na kusambaza mizigo, hatua inayotarajiwa kuunganisha masoko ya Afrika Mashariki na Kusini na Misri, Mashariki ya Kati, Asia na Ulaya.
Kuhusu kilimo, mifugo na uvuvi, Tanzania imeeleza fursa za ushirikiano na Misri katika umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu, uvunaji wa maji ya mvua, ufugaji wa kisasa na viwanda vya kuchakata mazao, huku ikikaribisha uwekezaji katika Ranchi ya Ruvu na ushirikiano na Jeshi la Kujenga Taifa, Magereza na Shirika la Chakula la Taifa katika miradi ya uzalishaji wa chakula.
Kwa upande wake, Rais El-Sisi amesema Misri iko tayari kushiriki katika mradi mkubwa wa kilimo utakaoshirikisha sekta binafsi ili kuimarisha usalama wa chakula.
Katika sekta ya elimu, Misri imeeleza utayari wa kutoa ufadhili kupitia Mpango wa Samia Scholarship katika fani za sayansi, tiba, akiliunde, TEHAMA na usalama wa mtandao, wakati katika afya imejitolea kujenga au kukarabati hospitali na kutoa mafunzo ya kibingwa katika upasuaji wa moyo, figo, ini na saratani.
Marais hao wameshuhudia utiaji saini wa hati mbili za makubaliano kuhusu ushirikiano katika nishati na uchukuzi, huku Rais Dkt. Samia akisisitiza hitaji la utekelezaji wa haraka wa makubaliano hayo.
Wakiwa wamefunga Jukwaa la Biashara na Uwekezaji, Rais Dkt. Samia amezialika kampuni zaidi za Misri kuwekeza nchini kutokana na mazingira rafiki ya biashara, akisisitiza kuwa mustakabali wa Afrika utajengwa na biashara za Afrika zinazowekeza barani humo.
Rais El-Sisi amesisitiza kuwa ushirikiano wa kiuchumi utaelekezwa katika miundombinu, teknolojia na kilimo huku sekta binafsi ikiongoza uwekezaji.
Kwa sasa, Misri inashika nafasi ya nane miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania, ikiwa na miradi 61 yenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 1.5, iliyozalisha zaidi ya ajira 4,000.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254








Post a Comment