" WATUHUMIWA 200 WAKAMATWA TANGA

WATUHUMIWA 200 WAKAMATWA TANGA

 


Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limesema limewakamata watuhumiwa 200 kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kujihusisha na makosa mbalimbali ya jinai kati ya Juni 1 na Julai 16, 2026, huku watuhumiwa 51 wakihukumiwa vifungo tofauti baada ya kupatikana na hatia Mahakamani kulingana na sheria za Nchi.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Julai 17, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi, ambaye pia amewaambia waandishi wa habari kuwa hali ya ulinzi na usalama mkoani humo ni shwari.

ACP Mchunguzi amesema watuhumiwa hao walikamatwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo dawa za kulevya, unyang'anyi, wizi, kupatikana na mali zinazodhaniwa kuwa za wizi, nyara za serikali, uharibifu wa miundombinu, noti bandia na makosa mengine ya jinai, akiongeza kuwa waliohukumiwa walipatikana na hatia ya makosa mbalimbali ikiwemo kulawiti, kubaka, kuzini na maharimu, kusafirisha dawa za kulevya, wizi wa mifugo na kuingia nchini bila kibali.

Amesema kuwa Julius Mustafa na Kilimo Issaya kila mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa ya kulawiti na kuzini na maharimu mtawalia, huku Sadiki Waziri akihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.

Katika operesheni dhidi ya dawa za kulevya, watuhumiwa 29 walikamatwa, ambapo 14 walikutwa na mabunda 750 ya mirungi yenye uzito wa kilogramu 45, huku wengine 15 wakikamatwa na bangi katika mfumo wa misokoto, pakiti, vifurushi na kete mbalimbali.

Kamanda huyo pia amesema pia watuhumiwa watano walikamatwa wakiwa na nyara za serikali na mali zinazohusiana na wanyamapori, huku vifaa vya miundombinu ya TANESCO na barabara, noti bandia za Kenya, televisheni 10, simu 25 na mali nyingine zinazodhaniwa kuwa za wizi vikikamatwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post