" BENKI KUU : PUUZENI UCHOCHEZI WA KUONDOA FEDHA BENKI

BENKI KUU : PUUZENI UCHOCHEZI WA KUONDOA FEDHA BENKI


Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewahimiza Watanzania wote kupuuza taarifa za upotoshaji zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii, zenye lengo la kuwachochea kuondoa fedha zao benki na kuzihifadhi majumbani.

Katika taarifa iliyotolewa karibuni jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Gavana wake, Bwana Emmanuel M. Tutuba, Benki Kuu imesisitiza kuwa taarifa zinazodai kuwa Benki Kuu inachapisha fedha kwa ajili ya kugharimia uchaguzi, au kwamba baadhi ya benki za biashara zimeishiwa fedha, ni za uongo na za uzushi kabisa.

"Napenda kuwafahamisha wananchi wote kuwa taarifa hizo siyo za kweli, zinapaswa kupuzwa na kukemewa wote wanaoupotosha umma kuhusu hili jambo. Tunawasihi wananchi kutokushawishika kutoa fedha zao kutoka kwenye mabenki," ilisema taarifa hiyo.

Uchapishaji Fedha ni Kisheria

Benki Kuu imefafanua kuwa, kama ilivyo kwa benki nyingine duniani, inachapisha fedha kwa mujibu wa Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu, Sura 197. Fedha hizo huwekwa kwenye mzunguko kulingana na shughuli za kiuchumi na mahitaji ya kubadilisha fedha zinazochakaa.

Kinyume na uchochezi huo, Benki Kuu imetoa takwimu thabiti kuonyesha utulivu na ustawi wa Sekta ya fedha:

Akiba ya Fedha za Kigeni: Imeongezeka hadi Dola za Marekani bilioni 6.7. Kiasi hiki kinatosha kuagiza bidhaa nje ya Nchi kwa kipindi cha miezi 5.4, ikilinganishwa na lengo la miezi 4.0.

Ukwasi na Mtaji: Viwango vya utoshelevu wa mtaji na ukwasi kwenye benki zote za biashara viko juu zaidi ya viwango vinavyotakiwa kisheria, ikiwa ni uthibitisho wa uthabiti wa sekta hiyo.

Hatari ya Kuzihifadhi Nyumbani

Benki Kuu imewaonya wananchi kuhusu hatari za kuondoa fedha na kuzihifadhi majumbani, ikisema kuwa hatua hiyo inawaweka katika hatari ya wizi, kupotea, kutumiwa vibaya, au uharibifu kutokana na majanga kama moto.

"Kutokana na mazingira hayo mazuri ya kiuchumi na kifedha nchini, uamuzi wa kuondoa fedha kutoka benki na kuzitunza nyumbani haufai kwa kuwa ni utamaduni wa kizamani wenye hatari nyingi ikilinganishwa na kuibwa, kuvutiwa wezi wanaoanza kukudhuru, kupotea, kuzitumia vibaya katika shughuli zisizokusudiwa," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

BoT imeongeza kuwa, uamuzi wowote wa kuondoa fedha benki na kuzihifadhi nyumbani unakinzana na juhudi za Serikali za kukuza matumizi ya mifumo rasmi ya kibenki.

Gavana Tutuba amewahimiza wananchi wote kuendelea kutumia huduma za benki bila wasiwasi wowote, na kuwataka wanaofanya upotoshaji huo kutambua kuwa wanachelewesha juhudi za Taifa za kuimarisha utulivu wa Sekta ya fedha nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post